Kigogo anaswa kwa tuhuma za uchawi kortini
Mtwara. Mmoja wa viongozi wanne wa vyama vya upinzani wanaokabiliwa na mashtaka ya kula njama, kutoa kauli za uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wananchi, jana alipekuliwa na polisi mahakamani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kufanya vitendo vya ushirikina katika eneo la mahakama.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni kumwona mshtakiwa huyo akimwaga kitu mithili ya udongo mbele ya mlango wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Mtwara.
Kitendo hicho kilimlazimisha hakimu anayesikiliza kesi ya viongozi hao kupita mlango wa uani.
Kwa upande wao, polisi waliokuwepo mahakamani walimkamata mshtakiwa huyo na kumtaka atoe nje mifuko ya suruali yake.
Hata hivyo mazingira hayakuruhusu na akaingizwa ndani na ambako walimkagua na kumkuta akiwa na kitu kinachofanana na unga mweusi kwenye mifuko ya nguo zake.
Polisi waliwamuru afagie vitu hivyo.
Viongozi wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Katani Ahmed Katani (33) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi na Hamza Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara.
Wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo, Katani aliunganishwa na Saidi Kulaga.
Baadaue mwendesha mashtaka aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kusikilizwa kwa kesi kwa madai ya kuwa upelelezi haujakamilika.
Wakili wa washtakiwa naye alikuwa na dharura na hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 25 mwaka huu.
Viongozi hao walipandishwa kizimbani kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara
chanzo:mwananchi
0 comments: