Mzee Small anateseka-1
Anachechemea huku mkono wa kushoto akiwa ameufumbata kwapani, uso umekumbwa na maumivu yanayoshindana na tabasamu hafifu analojaribu kulitoa. |
ANAFAHAMIKA zaidi kwa jina la Mzee Small, lakini jina lake halisi ni Small Wangamba.
Ana sifa nyingi, lakini iliyo kubwa ni ucheshi, uchangamfu, ukarimu na kila aina ya bashasha. Hata hivyo kwa sasa hali yake ni tofauti, mambo mengi yamebadilika.
Sipati shida kumpata pale nilipokusudia kumfikia na hata ninapofika nyumbani kwake katika banda la vyumba viwili ambavyo vimemalizwa kujengwa hivi karibuni, napokewa na msichana anayenikaribisha katika kiti nje ya kibanda hicho.
Ujumbe unapelekwa ndani kwa Mzee Small kuwa ana mgeni na dakika 20 baadaye mlango unafunguliwa, anachomoza mtu ambaye sipati taabu kumfahamu kuwa ni Mzee Small, mwigizaji nguli ambaye maradhi yamemkalisha kitako.
Anachechemea huku mkono wa kushoto akiwa ameufumbata kwapani, uso umekumbwa na maumivu yanayoshindana na tabasamu hafifu analojaribu kulitoa.
Hali hiyo inaakisi wimbo mmoja wa Shakila Abdallah ‘Bi. Shakila’ wenye mashairi ‘Macho yanacheka moyo unalia’. Kimsingi Mzee Small anaumwa ingawa anajaribu kutabasamu, kinachoonekana katika paji lake la uso ni tofauti na tabasamu hafifu analojaribu kulitoa pale macho yetu yanapogongana na wakati wa mazungumzo anabainisha kinachomsibu.
“Sipo vizuri, naumwa. Kwa sasa inawezekana ikaonekana kama nina nafuu kidogo, lakini naumwa,” anasema baada ya kunikaribisha katika chumba kimoja ambacho anakimiliki na mkewe.
Chanzo cha tatizo
Anasema tatizo lake lilimuanza Mei mwaka jana baada ya kurudi kutoka Mwanza alikokuwa na kazi ya kutumbuiza katika tamasha la kupambana na mauaji ya Albino. Tamasha hilo liliratibiwa na Kituo cha Under The Same Sun .
“Nilitoka Uwanja wa Ndege (Dar es Salaam) na kufika hapa nyumbani, nikaingia chooni moja kwa moja. Lakini wakati natoka, nikadondoka. Nilipojitahidi kunyanyuka haikuwezekana hivyo nikabebwa hadi chumbani,” anasema.
Anasema akiwa chumbani alijaribu kujinyanyua akajikuta anadondoka tena, hivyo akawahishwa hospitali moja jirani na nafuu haikupatikana.
Ikalazimika apelekwe Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam ambako alilazwa siku tatu kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
0 comments: