USHUHUDA WA WANACHAMA 5 WA CUF WAKIELEZA JINSI WALIVYOTESWA NA ASKARI HUKO MTWARA

 Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka (kulia) ni, Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Mtwara Mjini, Ismaili Njalu. Katibu wa Wilaya ya Mtwara mjini, Said Kulanga na Mwenyekiti wa Wilaya ya Mtwara mjini, Salum Mohamed wakiwaonesha waandishi wa habari majelaha waliyoyapata baada ya kupigwa na Wanajeshi wa Wananchi (JWTZ) katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Chama hicho Dar es Salaam.
CONTINUE READING
--------------
CHAMA cha Wananchi (CUF) kinaandaa utaratibu wa kufungua kesi mahakamani dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa watendaji wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi Mipango, Uchaguzi wa Bunge Shaweji Mketo,kwa niaba ya wanachama wenzake alisema, bado wanawasiliana na wanasheria, taasisi za haki za binadamu na mamlaka nyingine ili kupata mwongozo waweze kufungua kesi hiyo.

Mketo na wenzake watano, ni miongoni mwa watu walioonja joto ya mateso ya siku 28 kutoka kwa askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ambao wameweka kambi Mtwara kudhibiti machafuko yanayotokana na madai ya kuzuia bomba la gesi asilia lisijengwe Dar es Salaam.

Mbali na Mketo wengine ni Mwenyekiti wa Vijana Mtwara mjini Salum Mohamed, Mwenyekiti wa Mtwara mjini Salum Mohamed, Mwenyekiti wa Wilaya Mtwara vijijini Ismail Jamal,Katibu wa Wilaya Mtwara mjini Said Kulaga na dereva wa CUF makao makuu Kashinde Juma.


Naibu Mkurugenzi Uchaguzi na Mipango wa CUF, Shaweji Mketo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kuteswa kwa wanachama watano wa chama hicho na askari wa JWTZ mkoani Mtwara. 
 -----
Akisimulia mkasa huo uliompata yeye na wenzake alisema wakiwa njiani walikutana na gari mbili za jeshi kubwa na ndogo zikiwa njia panda ya newala na mtwara mjini,na kuwasimamisha huku walitokea askari wapatao 50 vichakani na kuanza kuwapiga huku wakiwasachi mifukoni.

“Askari wa JWTZ walikuwa 50 walitusachi na kuchukua fedha zangu shilingi 85,000 na nilipoanza kuzuia fedha hizo wasizichukue ndipo walipoanza kunipiga kweli wakanivua viatu vyangu nilivyowahi kununua nje ya nchi wakavichukua na mimi kuniachia vyao vya jeshi hivi hapa ,”alieleza Mketo.

Alisema walikuwa wakipigwa na fimbo, kumwagiwa maji yaliyokuwa yamewekwa barafu na pilipili jambo ambalo liliwafanya waendelee kupata maumivu makali sana.

Mketo alisema hata hivyo kuteswa kwao ni ishara kuwa Mtwara bado inanuka damu na hakuna usalama huku wananchi wengi wakihofiwa kufariki dunia.

Hata hivyo alisema wakati wakiendelea kuwatesa alisikika mwanajeshi mmoja akisema wao wapo pale kwa ajili ya kutekeleza amri ya Waziri Mkuu aliyoitoa Bungeni kwamba wananchi watakaokaidi amri ya serikali wanatakiwa kupigwa.

Kiongozi huyo ambaye aliongea kwa masikitiko makubwa huku akiwataka wenzake kuonesha majereha kwa wanahabari alisema kuwa licha ya kuwaambia wanajeshi waliokuwa wakiwatesa kuwa amefanyiwa upasuaji mkubwa wasimpige eneo hilo hawakujali kwani waliendelea kumchapa na bakora katika eneo la mshono hadi lilipogeuka rangi na kuwa nyeusi.

Alisema kiongozi mmoja ambaye ni Mwenyekiti wa Mtwara mjini Salum Mohamed aliambiwa azivute ndevu zake kwa kutumia mikono na alifanya hivyo hadi haapo zilipoanza kuvuja damu ndipo wakamwambia walichokuwa wanakihitaji.

Mketo alisema vitendo hivyo ni vya kinyama na kwamba haviwezi kuvumilika hivyo serikali inatakiwa kuviangalia utendaji kazi wa vyombo vya dola kwani ni kulinda raia na si kutesa.

Hata hivyo aliilaumu serikali kwa kuvifungia vyombo vya habari mkoani humo kwa kigezo cha kwamba vinawashawishi wananchi kuandamana jambo ambalo si kweli.

0 comments: