SIMULIZI : 'TULIVYONUSURIKA KUUAWA NA POLISI KATIKA MKUTANO WA CHADEMA ARUSHA'.....SOMA MWENYEWE HAPA
Ilikuwa Juni 18, mwaka huu katika Uwanja wa Soweto  wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  walikukusanyika ili kuwaaga watu wanne waliokufa kufuatia bomu  lililolipuka Juni 15, katika uwanja huo.
Tangu bomu hilo lilipolipuka  siku  hiyo  (Jumamosi), viongozi wa Chadema akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe  walifanya mikutano uwanjani hapo Juni 17 na 18, Japo tayari polisi  walishazungusha utepe katika eneo lililolipukia bomu.
Siku hiyo, saa 9 alasiri wakati mkutano ukiendelea  na viongozi wa chama hicho wakitoa maelekezo ya jinsi ya kuaga maiti,  polisi waliokuwa wamefurika eneo hilo waliwashambulia kwa mabomu ya  kutoa machozi ili kuwatawanya.
Malisa anayeishi Kata ya Ngarenaro jijini humo  alifika uwanjani hapo kumwokoa baba yake Godwin Malisa ambaye ni  mlemavu, alijikuta akipata kipigo cha mbwa mwizi.
“Nilikuwa namfuata baba yangu ambaye ni kada wa  Chadema. Kutokana na ulemavu wake nilihofu angepata matatizo kama vurugu  zingezuka,” anasema Wema na kuongeza:
“Nilikuta uwanja ukiwa umefurika wananchi  wakiwasikiliza viongozi wa Chadema. Viongozi hao ni Mbunge wa Arusha  Mjini, Godbless Lema ambaye alihutubia na kumwachia Tundu Lissu (Mbunge  wa Singida Mashariki) naye akamwachia Said Arfi (Mbunge Mpanda Kati).  Alipomaliza kuwataka wanachama hao waelekee Hospitali ya Mount Meru,  ndipo mabomu yakaanza kulipuliwa.”
Anaendelea kusema: “Nilimwambia baba tuondoke  lakini tulikuwa tumeshachelewa, kwani polisi walikuwa wametuzingira.  bomu la pili liliangukia mbele yetu. Askari mmoja akasema ‘laleni  chini’, tukalala tukidhani tutakuwa salama. Lakini walikuja askari na  kutupiga marungu mwili mzima mimi na baba,”
“Ghafla akatokea askari mwingine akawakataza  wasitupige, tukadhani tumeokoka. Mara wakatokea askari wengine, hapo  ndipo kilikuwa kipigo kitakatifu. Nilijaribu kuwazuia wasimpige baba kwa  kuwa ni mlemavu, wakanikebehi kuwa huyo ni hawara yangu. Walinipiga  mpaka mkono na mguu ya kushoto ikavunjika.
“Tulikuwa kwenye kibaraza cha nyumba wakati askari  wanatupiga. Askari mmoja alirarua gauni langu chini na juu, hadi  nikabaki uchi mbele ya baba. Mwingine akakoki bunduki na kuielekeza  katikati ya mapaja yangu ili alipue sehemu za siri, wenzake wakamkataza.  Mwingine alisema kuwa atanibaka. Baba alinikumbatia akasema watuue  wote, mimi niliomba wasituue maana nimeacha mtoto mchanga nyumbani.”
Anasema askari walikuwa wakimbeza kwa kumuuliza kwa nini yeye ni  mwanachama wa Chadema.
“Walisema ‘unajifanya wewe Chadema, sasa ndiyo  utajua kuwa CCM inatawala. Chezea CCM wewe.’ Mimi niliwaambia sina chama  chochote nimekuja kumwokoa baba yangu. Wakati huo wote walishanivua  hereni, simu wakachukua na fedha zilizokuwa ndani ya pochi na kuitupa  chini ikiwa tupu.”
Maelezo ya baba yake
Kauli ya Serikali
Hata hivyo Wema anasema alikuja askari wa kike aliyekuwa akipiga  picha za matukio na kuwasaidia. Wakati huo watu wote wameshatawanyika  uwanjani hapo na askari wameshaanza kujipanga baada ya kuitwa kwa  filimbi.
“Alitusikitikia na kusema, ‘kwa nini  mnang’ang’ania kuwa Chadema? Angalieni sasa mlivyoumia na viongozi wenu  wamewakimbia.’ Akaokota kanga iliyoachwa uwanjani na kuja kunifunika,”  anasema na kuongeza:
“Kisha likaja gari la polisi tukabebwa na  kuingizwa humo. Mwendo tuliondoka pale ulikuwa wa kasi huku wakiendelea  kulipua mabomu na kutukanyaga bila kujali. Tulishtukia tuko Hospitali ya  Mount Meru, tukabwagwa hapo na gari hilo likaondoka.”
Wema anasema walitibiwa kwa siku kadhaa kabla ya kuruhusiwa ili kuugulia nyumbani.
Maelezo ya baba yake
Baba yake Wema, Godwin Malisa japo hakupata majeraha makubwa, anaendelea kuugulia maumivu makali ya mwili mzima.
“Kilichonisikitisha ni kitendo cha kumpiga na  kumdhalilisha mwanangu mbele yangu. Askari wengine walikuwa wakijaribu  kuvunja hili gongo ninalotembelea kwa sababu ya ulemavu,” anasema Malisa  na kuongeza:
Alalamikia kauli ya Pinda
“Nimesikitishwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo  Pinda aliyoitoa hivi karibuni Bungeni Dodoma ya kuwataka askari  waendelee kupiga wananchi. Kwa hali hii sisi wanyonge natuna pa  kukimbilia.”
Akisimulia zaidi, Malisa anasema, siku hiyo licha  ya watu kuwa wengi katika uwanja huo, Jeshi la Polisi halikufuata kanuni  zake za kutoa ilani kwa wananchi kabla ya kuanza kushambulia.
Licha ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha kusema  hakukuwa na majeruhi siku hiyo, inaelezwa kuwa wengi walijeruhiwa kwa  kupigwa na polisi.
Kauli ya Serikali
Akijibu maswali ya  wabunge hivi karibuni bungeni mjini Dodoma,  Waziri Mkuu Mizengo amewahimiza polisi kuendelea kuwapiga wananchi  wanaokiuka sheria, kwa kuwa nchi inafuata utawala wa sheria.
“Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki wewe  ukakaidi, utapigwa tu...Maana hakuna namna nyingine. Maana lazima wote  tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.  Sasa  kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba wewe ni imara zaidi, ni jeuri,  watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu kwa sababu hakuna nyingine eh…  maana tumechoka sasa.”
SOURCE : Mwananchi Monday 24 June, 2013
SOURCE : Mwananchi Monday 24 June, 2013

0 comments: