VITA YA NGUMI KATI YA RAY KIGOSI VS ZITTO KABWE NA HALIMA MDEE VS JACKLINE WOLPER YAKARIBIA
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzania Bungeni, vilevile akiwa Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, ameshaongea mengi kuhusu nafasi yake ya kumchapa Ray ambaye naye amesema hawezi kupoteza pambano hilo.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, ameapa kupiga ngumi adimu na kumchakaza staa wa filamu Tanzania, Jacqueline Wolper.
Vilevile, Mbunge wa Viti Maalum (Vijana), Mkoa wa Mara kwa tiketi ya CCM, Ester Bulaya, atakuwa na kazi moja tu siku hiyo ya kutoana ngeu na mtaalam wa kucheza na kamera, Aunt Ezekiel.
Kuhusu jinsi wanavyojianda, soma tambo zao kila mmoja kwenye boksi lake:
HALIMA MDEE
Inaonekana Wolper hajawahi kupigwa, hii ni mashine kubwa sana. Kifua changu ni chepesi sana kwa sasa kutokana na mazoezi ninayofanya. Nina uhakika ngumi yangu moja tu itampeleka chini na mchezo utaishia hapo, kwa hiyo madaktari wampime afya mapema, nisije kuua.
ZITTO KABWE
Nimetoka jeshini hivi karibuni na nimefuzu kwa alama nzuri sana, hili suala Ray inabidi aliangalie kwa umakini. Mimi ni bondia mzuri sana, nitamchapa na hatamaliza raundi ya pili. Nafanya mazoezi mazito, najitesa kwa ajili yake.
WOLPER
Nimetoka Afrika Kusini juzijuzi kwa ajili ya kujiandaa na pambano langu na mheshimiwa Mdee. Nimekuwa nikimtamani kwa muda mrefu, sasa arobaini yake itafika Julai 7 pale Uwanja wa Taifa. Nawaomba radhi wananchi wa Kawe kwa sababu nitauweka pembeni uheshimiwa wake halafu nitampiga mbunge wao.
ESTER BULAYA
Mimi ni mtu wa Mara na kila mtu anajua watu wa Mara tupoje kwenye upande wa mkono. Aunt Ezekiel ajipange kisawasawa kwa sababu nimejiandaa kumkalisha raundi ya kwanza. Nitamuonesha siku hiyo kuwa mbali na ubunge, mimi ni bondia kamili ninayeweza kupigana ngumi za kulipwa.
RAY
Sipendi Zitto aone mazoezi yangu, ataogopa. Vifaa ninavyotumia kujiandaa na pambano lake ni vizito tena adimu sana. Nataka ajue kwamba nitampiga. Ni mheshimiwa, namheshimu sana ila pale ulingoni itabidi nimchape.
AUNT EZEKIEL
Salaam kwa mheshimiwa Ester Bulaya, nataka ajue kuwa mimi ngumi zangu ni nzito sana. Nawaomba watu wa huduma ya kwanza waweke karibu ambulance wakati nitakapopanda ulingoni, ngumi yangu moja itampeleka sakafuni na hatanyanyuka. Hivi sasa nimejichimbia, nikiibuka nitakuwa tayari kwa ajili ya kutoa dozi.
0 comments: