"ACHENI KUFUATILIA VIMINI VYANGU "- MKE WA OBAMA
Michelle Obama na Laura Bush walikuwa kivutio jana  kwenye Mkutano wa wake wa marais wa Afrika unaoendelea Dar es Salaam,  pale walipoongelea kwa mzaha jinsi vyombo vya habari vinavyoshupalia  kuandika kuhusu staili za nywele na  mavazi ya wake wa marais, huku  vikiacha masuala ya msingi.  
 
Mkutano  huo uliofunguliwa jana na Rais Jakaya Kikwete, ni maalumu kwa ajili ya  kusaidia wanawake wajasiriamali wa Afrika, unatarajiwa kumalizika leo.
Wakizungumza  kwenye mjadala ulioongozwa na Mwandishi wa Habari wa Marerkani, Cokie  Roberts,  Michelle, ambaye ni mke wa Rais wa Marekani, Barack Obama,  alisema alifurahia kupata nafasi ya kufanya majadiliano na Laura, ambaye  ni mke wa Rais wa zamani wa Marekani.
“Ninampenda mwanamke huyu,” alisema Michelle kwa utani kama vile hamfahamu.  
 “Sishangai  sana maana tuko klabu moja nadhani,”  alijibu Laura kwa utani akiwa na  maana kuwa,  wao wote wana uzoefu wa kuwa wake wa marais.
“Unajua  tunaishi maisha ya shida, maana wenzetu wa habari wanaangalia zaidi  staili za mavazi na nywele zetu badala ya kuangalia mambo ya msingi,”  alisema Michelle.
 Alisema  mwanzoni mwa mwaka huu, alibadili staili ya nywele lakini alishangaa  jinsi suala hilo lilivyokuzwa na vyombo vya habari.
“Watu  wanapaswa kuelewa, wake za marais nao hufanya mambo mazuri ya jamii na  kazi yao siyo kubadili staili za nywele na mavazi tu,” alisema Michelle,  ambaye anasifiwa na majarida mbalimbali ya Marekani na Ulaya kwa  mitindo yake ya mavazi na nywele.
“Nadhani ndugu zetu wanahabari watabadilika,” alitania Laura wakati wa mjadala huo.
Cherie Blair 
Naye  Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, Cherie, jana  alitangaza mpango wa kuwasaidia wanawake wa Afrika kufanya biashara kwa  kutumia mawasiliano ya simu.
Mpango huo unasimamiwa na Taasisi ya Cherie Blair Foundation kwa kushirikiana na Kampuni ya ExxonMobil.
Akitangaza mpango huo kwenye mkutano wa wake za marais wa Afrika, Cherie alisema watatoa mafunzo ili kufanikisha mkakati huo.
Cherie, ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, alisema  wameanza utekelezaji wa mpango huo nchini Tunisia.

0 comments: