ASUSIWA MAITI YA KICHANGA CHA MIEZI SABA SEBURENI KWAKE
DEREVA wa daladala aliyefahamika kwa jina la Aswile Mwalukoba, 45, amesusiwa maiti ya mtoto wa miezi saba baada ya kudaiwa kumpa mimba mwanafunzi kisha kumtelekeza.
Tukio hilo lilitokea hivi karibunu katika eneo la Mama John, Mtaa wa Ihanga, Kata ya Ilomba jijini hapa baada ya binti aliyefahamika kwa jina la Carolina Kyando ambaye alikuwa akisoma masomo ya jioni katika Shule ya Juhudi kupewa mimba na kutelekezwa, kisha mtoto aliyejifungua kuugua kwa muda mfupi na kufariki dunia.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Mtaa wa Ihanga, Emmanuel Mwasibata alisema kutelekezwa kwa maiti ya mtoto huyo kulitokana na dereva huyo kugoma kuuzika mwili huo kwa kile alichodai kuwa hivi sasa haishi na binti huyo waliyeachana muda mrefu.
Calorina alipoulizwa sababu ya kuupeleka mwili wa mwanaye kwa Mwalukoba, alidai ni kutokana na mzazi mwenzake huyo kuwatelekeza.
“Mara baada ya mtoto huyu kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospital ya Igawilo nilimpigia simu mzazi mwenzangu kwa lengo la kumpa taarifa ya msiba.
“Baada ya kumfahamisha alisema yuko tayari kwa ajili ya maziko ya mwanaye na anafanya taratibu za kuwasiliana na ndugu zake walioko Tukuyu, ajabu ni kwamba kesho yake akawa hapatikani kwa simu wala nyumbani kwake akawa haonekani
“Kwa kushirikiana na majirani zake waliopigwa na butwaa kuhusiana na tukio hilo, tuliuchukua mwili wa mtoto hospitali hadi kwake ambapo tuliiweka maiti kwenye kiti tukawa tunamsubiri arudi kutoka alikokwenda, kesho yake alirejea akiwa na mdogo wake Gabriel,” alisema Carolina.
Mwenyekiti wa Mtaa, Mwasibata alipomhoji juu ya kutoweka kwake nyumbani kwa siku mbili huku kukiwa hakuna mawasiliano yoyote alidai alikwenda kuwataarifu ndugu zake.
Mwasibata alisema kilifanyika kikao cha usuluhishi ambapo aliomba radhi na akakubali kumzika mwanaye.
Mazishi ya mtoto huyo yalifanyika katika Makaburi ya Iyela jijini hapa saa 12 jioni wiki iliyopita na kuhudhuriwa na ndugu wa familia zote mbili.
0 comments: