"WAKATI KIKWETE AKIONGOZA KUOMBA KONDOMU KWA OBAMA, MAGAZETI NAYO YALIISHIA KUANDIKA HABARI YA KUSHIKANA VIUNO".... GODBLESS LEMA
CHAMA cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuanza kutoa mafunzo ya kujihami kwa vijana wao maarufu kama Red brigedi kuanzia Agosti mosi, mwaka huu.
Akitangaza tarehe hiyo jana wakati wa mkutano wa chama hicho uliofanyika Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini, kiongozi wa ulinzi wa chama hicho kanda ya Nyanda za juu kusini Lucas Mwampiki, alisema kuwa ameamua kuweka wazi adhima hiyo ili serikali isiendelee kusumbuka kuwa inao uwezo wa kuwazuia.
‘’Polisi msisumbuke kutafuta kuwa tutaanza lini, ni hivi, tutaanza tarehe 1, mwezi wa nane mwaka huu’’ alisema Mwampiki ambaye pia ni diwani wa kata ya Mwakibete Jijini Mbeya.
Mgeni rasmi katika mkutano huo Godbless Lema ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na Mbunge wa Arusha mjini, alisema amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa vijana waliohitimu mafunzo ya JKT na kuachwa bila ajira ili wajiunge na mafunzo hayo.
‘’Nimekuwa nikipokea simu nyingi za vijana waliohitimu JKT na kuachwa mitaani wakiomba kujiunga na mafunzo ya Redbrigedi huku wakiuliza kiingilio’’ alisema Lema.
Alisema kuwa ijulikane kuwa mtu anapozuia demokrasia anazalisha waasi na Chadema hawapo tayari kuuawa kijinga.
Mbali na suala hilo, Lema alisema alishangazwa na uandishi wa vyombo vya habari hapa nchini katika ujio wa Rais wa Marekani Barack Obama, ambapo Magazeti mengi yaliandika habari za kushikana viuno na mkewe badala ya kuandika jambo ambalo aliloijia.
‘’Waandishi wa Tanzania badala ya kuandika alichojia Obama, wao waliishia kupiga picha akiwa ameshikana na mkewe na kuweka front page huku madini yakiondoka na Rais Kikwete akiongoza kuomba Kondomu na kusaini mikataba ya kutorosha madini yetu’’alisema Lema huku akishangiliwa na wananchi zaidi ya 2000 waliohudhuria mkutano huo wakiwemo viongozi wa CCM.
Aliwaambia wanachama wa Chadema kuwa waache kuwachukia wanachama wa CCM bali wawaelimishe taratibu maana hata ukitaka kupata kifaranga huwezi kununua yai dukani na kulipasua kisha ukapata kifaranga bali mpaka yai hilo liatamiwe na kuangaliwe.
Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi, alisema kwa sasa anakubali kuwa yeye ni ‘’Rais wa Mbeya’’ kutokana na wananchi kumkubali na kwamba CCM wasitarajie kulikomboa Jimbo la Mbeya Mjini mwaka 2015 na aliwashukuru sana Polisi wa Mbeya kwa kuacha kuisaidia CCM.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo wa kuimarisha chama katika kata ya Nsalala na Utengule Usongwe Kissman Mwangomale (KK) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mshikamano kata ya Nsalala, alisema kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kujiuzulu kwasababu alitamka kuwa amechoka.
‘’Pinda anapaswa ajiuzulu maana alitamka kuwa amechoka, sisi hatujachoka tuna uwezo wa kuongoza dola aachie ngazi au afute haraka kauli yake’’ alisema Mwangomale.
Naye diwani wa kata ya Iyela ya Jijini Mbeya Charles Mkela, aliwashukuru wanachama wa CCM kumpigia kura nyingi za ndiyo katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni na kukiwezesha Chadema kushinda.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwemo Frank Mwaisumbe ambaye ni Mratibu wa Chadema kanda ya nyanda za juu kusini na viongozi kutoka Mbeya mjini na wilaya ya Mbozi.
0 comments: